Wednesday , 6th Nov , 2024

Kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini, unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, waandishi wa habari nchini wametakiwa kujiweka mbali na mapenzi ya chama chochote cha siasa ili waweze kufanya kazi bila kukutana na changamoto.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa  Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile, wakati anaongea na wanahabari kuelekea mkutano mkuu wa jukwaa hilo utakaokutanisha wahariri zaidi ya 100 kutoka kila kona ya nchi yetu.
“Ifikapo Novemba 27, watanzania watakuwa wanashiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, sasa miongoni mwa mada ni kwa namna gani wanahabari tutashiriki uchaguzi huu kwa kuzingatia haki na ukwei kwenye kuripoti, lakini pia tujiepushe na kuvaa sare za chama cha siasa ili tuweze kufanya kazi zetu bila kukutana na chanhamoto wakati wa kuripoti”, DEODATUS BALILE-Mwenyekiti TEF.

Aidha Balile anaelezea ajenga zitakazozungumziwa kwenye mkutano mkuu wa Jukwaa la wahariri nchini.

“Miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa kwenye mkutano huo ni pamoja na kuingiza wanachama wapya 24, utendaji wa vyombo vya habari, uchumi wa vyombo vya habari, mabadiliko ya Teknolojia na ufatiliaji wa maadili, sheria na miiko ya uandishi wa habari”, DEODATUS BALILE-Mwenyekiti TEF.

Nae mjumbe wa kamati tendaji ya jukwaa hilo, Salim Salim , anawakumbusha waandishi wa habari kuzingatia maadili wakati wa utekelezaji wa majukumu yetu.
“Kuwa na hekima wakati unamfanyia mtu interview haitakupunguzia kitu, tabia kuna muda unaona aibu baadhi ya waandishi wanafanya, msikubali kipato kiwe sababu ya utu wako kuwa chini, tusaidiane na mavazi yaendane na na kazi zetu lakini pia tujiendeleze kimasomo”, SALIM SALIM-Mjumbe wa Kamati tendaji TEF.