Tuesday , 29th Oct , 2024

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani NECTA.Dkt.Said Mohamed, ametangaza matokeo ya darasa la saba ambapo  ufaulu wa jumla umeongezeka huku ubora wa wanafunzi waliopata madaraja A na B ukiimarika zaidi

“Jumla ya watahiniwa 974,229 Sawa na 80.87%, watahiniwa wenye matokeo wamefauli na kumaliza Elimu ya Msingi 2024, hivyo ufaulu wa jumla umeongezeka kwa 0.29, Kati ya watahiniwa hao wavulana ni 449,057 Sawa na 81.85% na wasichana ni 525,172 Sawa na 80.05%, hivyo ufaulu wa wasichana umeshuka kwa 0.53% na ufaulu wa wavulana umeongezeka kwa 1.26%”

“Ubora wa faulu kwa watahiniwa waliopata madaraja ya A na B umeimarika ambapo watahiniwa 431,689 sawa na asilimia 35.83 wamepata madaraja ya A na B ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.65 ikilinganishwa na mwaka 2023. Kati ya watahiniwa 431,689 waliopata ubora wa ufaulu katika madaraja ya A na B, Wasichana ni 216,568 (33.01%) wakiwa na ongezeko la asilimia 9.09 na Wavulana ni 215,121 (39.21%) wakiwa na ongezeko la asilimia 8.28 ikilinganishwa na mwaka 2023”

Katika matokeo hayo pia yameonesha kuwa wasichana wameongoza zaidi katika somo la Kiswahili huku ufaulu wa somo la English Language nao ukiendelea kuimarika

“Ufaulu wa somo la Kiswahili ni muri ambapo asilimia 86.58 ya watahiniwa wamefaulu. Katika somo la English Language ufaulu umeendelea kuimarika kwani asilimia 43.48 ya watahiniwa wamefaulu ambapo ufaulu wa somo hilo umeongezeka kwa asilimia 9.13” 

"Ufaulu wa Wavulana na Wasichana katika somo la Kiswahili na English Language unawiana kwani Wasichana wamefaulu zaidi kuliko Wavulana kwa asilimia 0.36 katika somo la Kiswahili na katika somo la English Language Wavulana wamefaulu zaidi kuliko Wasichana kwa asilimia 0.25."

"Ubora wa ufaulu unaonesha kuwa, watahiniwa waliopata madaraja ya A na B katika somo la Kiswahili ni asilimia 53.46 ikilinganishwa na asilimia 69.41 katika mwaka 2023. Katika somo la English Language watahinia waliopata madaraja hayo ni asilimia 15.25 ikilinganishwa na asilimia 11.40 katika mwaka 2023" Dkt. Said Mohamed, Katibu Mtendaji NECTA.

Katika hatua nyingine Baraza hilo limeyafuta matokeo ya watahiniwa 45 ammbao walibainika kufanya udanganyifu 

"Baraza la Mitihani la Tanzania limefuta matokeo yote ya watahiniwa 45 ambao walibainika kufanya danganyifu katika Mtihani kwa mujibu wa Kifungu cha 5(2)j) cha Sheria cha Baraza la Mitihani Sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu 30(2)(b) cha Kanuni za Mitihani za Mwaka 2016, pamoja na watahiniwa 16 walioandika lugha ya matusi katika skripti zao kwa mujibu wa Kifungu cha 17(1) cha Kanuni za Mitihani za Mwaka 2016,  Dkt. Said Mohamed, Katibu Mtendaji NECTA.