Monday , 28th Oct , 2024

Wananchi kutoka nchi za Afrika Mashariki wameomba Serikali kurudisha Taasisi za Fedha za Serikali ili ziweze kuwafikia wananchi wengi waishio vijijini Kwani taasisi zilizopo zimelenga zaidi kupata faida na sio kuwekeza kwa wananchi waishio vijijini.

Ombi hilo limetolewa baada ya kuonekana huduma nyingi za kifedha kupatikana maeneo ya mijini na sio kila sehemu nchini na kusababisha baadhi ya makundi ya watu kukosa huduma hiyo muhimu.

"Ni lazima tuhakikishe Serikali inakuwa na taasisi zake za kifedha ili iweze kwenda vijijini ili iweze kuwafikia wakulima, tukitegemea hizo tu tunazosema binafsi, hawawezi kwenda kule kwa sababu wanaangalia faida ila kwa mkulima ukiangalia kipato chake atawezaje , kahiyo Serikali ihakikishe tunarudi nyuma kidogo lakini sio kurudi nyuma ni kwenda mbele kuhakikisha kuwa kunakuwa na taasisi ambazo zinahudumia jamii mbalimbali za vijijini kama vile ya wakulima, wafugaji n.k", Prof. Humphrey Moshi-Mkazi wa Dar es Salaam.

"Wanapaswa kusaidia umma miundombinu ambapo tutaweza kupata huduma za mtandao, maunganisho mengi, huduma ya simu janja nyingi ambapo watu wataweza kufanya huduma za kifedha za mtandaoni, lakini pia Serikali iwekeze kwenye Elimu, kuwelimisha wanawake , watoto na kila mtu namna bora wanaweza kunufaika na huduma za kifedha",Anne Kamau-Mwananchi kutoka Kenya.

Nchi za jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki zimekutana jijini Dar es Salaam  kwa ajili ya kujadili ni kwa namna gani tafiti zinaweza kusaidia watu na wananchi wa kawaida kuibngia katika mifumo ya kifedha, na hapa Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya utafiti uchumi Africa, anaelezea malengo ya kongamano hilo.

"Kufanya biashara tunayotaka lakini pia kuwatumia hela watoto shuleni , huduma za fedha ziweze kupatikana kwa kila mmoja kwa wakati sahihi , kiasi halisi na tukiweza kufanya kwa njia ya dijitali na kupunguza gharama hautahitajika kwenda benki ndio upate fedha, unakaa hapa unatuma fedha unaamka saa8 usiku unatuma hela na hiyo ndio tunahitaji kwa kila mtu", Prof. Victor Murinde-Mkurugenzi Mtendaji AERC.

Kwa upande wake Mbunge wa Bunge la Afrika mashariki, Abdullah Makame, anasema kupitia kongamano hilo wanakuja na maazimio yatakayosaidia kuboreha huduma za kifedha kwa wananchi wa Afrika Mashariki.

"Benki hizi nyingine zinashindwa kufika katika maeneo ambayo yako vijijini huko lakini vilevile ukija katika mfumo wa kidijitali, si kila mtu ana simu na sio kila mwenye simu ana simu ambayo ina mtandao kwahiyo tunasema kwamba hizi simu na mtandao viweze kila mtu kupata huduma hizi za kifedha ziweze kumfikia kila mtu kwa lengo la kuboresha maisha ya watu wa Afrika mashariki." Abdullah Makame -Mbunge Bunge la Afrika mashariki.