Sunday , 20th Oct , 2024

Moussa Camara amefanya makosa katika michezo miwili mfululizo ambaye imeathiri timu ya Simba kwa kusababishia kudondondosha alama ambazo zinawapa faida Mpinzani wake katika mbio za Ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara. Mchezo dhidi ya Coastal Union na jana kwenye chezo wa Dabi dhidi ya Yanga.

Moussa Camara Golikipa mpya raia wa Guinea alibeba matumaini makubwa ya Wana Msimbazi kwa kupata Mlinda Mlango ambaye anauwezo wa kucheza mpira kwa miguu yake. Katika michezo miwili mfululizo nyota huyo amefanya makosa ambaye yameigharimu klabu ya Simba alama 5 ambazo zinaweza kuwa alama muhimu kwenye mbio za ubingwa wa ligi kuu ambao timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi Karikaoo imeutafuta kwa misimu mitatu mfululizo bila mafanikio.

Klabu ya Wekundu wa Msimbazi siku ya jana Oktoba 19, 2024 ilipoteza mchezo wa Dabi mbele ya Watani wao wa jadi kwa kufungwa goli 1-0. Goli ambalo kwa kiasi kikubwa lilichangiwa na makosa ya Mlinda mlango wao raia wa Guinea Moussa Camara ambaye aliruka kuudaka mpira uliokuwa unaelekea nje na kuurudisha uwanjani na kumkuta Kiungo wa Ushambuliji wa Yanga raia wa Congo DRC Maxi Nzengeli aliyepiga mpira uliomshinda beki Kelvin Kijili na kuuelekezea kwenye goli la timu yake.

Camara amefanya makosa katika michezo miwili ya ligi kuu Tanzania bara ambayo imesababisha Simba SC kudondosha alama 5 ambazo zinaweza kusababisha faida kwa Wapinzani wao katika mbio za ubngwa wa ligi kuu ya Tanzania. Sehemu ambayo huwa haiitaji mbwembwe uwanjani ni eneo la Golikipa kwani makosa yake huisababisha goli hivyo kupelekea timu kupoteza mchezo.

Mchezo dhidi ya Coastal Union kutoka Tanga uliochezwa kwenye uwanja wa KMC Complex Spider Man wa Simba alijisahau akitoka langoni na kushindwa kuokoa mpira uliopigwa na Mchezaji wa Wagosi wa Kaya na kuufanya mchezo kumalizika kwa sare ya kufungana goli 2-2 na kudondosha alama mbili. Jana mchezo mkubwa katika mpira wa Tanzania dhidi ya Mtani wao wa Jadi anafanya kosa jingine linalopelekea kupoteza mchezo kwa kufungwa 1-0 hivyo kuifanya timu ya Simba SC kupata alama 1 katika alama 6 iliyopaswa kuzipata katika michezo miwili.

Mashabiki wa Simba na Yanga wanasamehe mambo mengi sana kwa Wachezaji lakini si kufanya makosa ambayo husababisha kupoteza mchezo dhidi ya Wapinzani wao wa Jadi, mchezo wa Dabi ya Kariakoo ni sehemu pekee ambayo Mchezaji anaweza akawa Shujaa ama adui wa Mashabiki kwani mchezo huu hubeba maisha ya Watu.

Camara inawezekana Wanasimba wakakusamehe makosa yako dhidi ya Coastal Union ila kosa ulilofanya dhidi ya Yanga ni kosa ambalo linaweza kukusababishia ukauchukia jumla mpira wa Tanzania. Simba SC ni bora ikafungwa na Lipuli ya Iringa lakini si timu ya Wananchi ukizingatia kosa lako limefanya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kupoteza mchezo wa nne mfululizo mbele ya Mahasimu wao wakubwa timu ya Yanga.

Nakukumbusha tu Moussa Camara Tanzania ukitaka kuwa Shujaa basi hakikisha unashinda mchezo dhidi ya Mtani wako wa Jadi kosa lako la jana linaweza likawa limebebea tiketi yako ya kurudi kwenu pindi ambapo Ayoub Lakred atakapopona.