Kuelekea dabi ya Kariakoo Oktoba 19, 2024 Beki kisiki wa timu Yanga Ibrahimu Abdullah Hamad maarufu kama Bacca amemtumia salamu Mshambuliaji wa timu ya Simba Lionel Ateba kwa kumwambia wataonana uwanjani tarehe 19. Ateba wiki iliyopita alizungumza kwenye siku ya Vyombo vya Habari kwa Timu za Ligi kuu Tanzania bara kwamba haoni Mlinzi wa kumzuia kufunga siku ya dabi kutoka kwenye kikosi cha Wapinzani wao siku hiyo kikosi cha Yanga kinachonolewa na Mwalimu Miguel Gamondi.
Joto la mchezo mkubwa ambao huteka hisia na akili ya Mashabiki na Wapenzi wa mpira wa miguu Tanzania kama si Afrika Mashariki. Tambo za Wachezaji zimeanza kumiminika na kuelekea mtanange huo Beki kisiki wa timu ya Wananchi Ibrahimu Bacca yeye ametamba kwa kusema anamsubiri Lionel Ateba Mshambuliaji wa Wekundu wa Msimbazi kwa hamu.
Ateba alitamba siku ya Vyombo vya habari kwa vilabu vinavyoshiriki ligi kuu Tanzania bara, Mkameruni wa Simba alisema atafunga siku ya mechi ya Watani wa Jadi Dabi ya Kariakoo siku ya Oktoba 19 mchezo utakaopigwa uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar es salaam. Mshambuliaji huyo mwenye nguvu na uwezo mkubwa wa kufumania nyavu ameweka ahadi ya kufunga siku ya mchezo huo kwa kusema hakuna Mlinzi wa kumzuia yeye asifunge kwenye kikosi cha Yanga.
Yanga imekuwa na muendelezo mzuri wa kimatokeo dhidi ya Wapinzani wao hao, katika michezo mitatu mfululizo wa hivi karibuni timu ambayo ni Mabingwa watetezi wa ligi ya Tanzania wameshinda mechi zote tatu. Mchezo ambao ulizua mtafaruku kwenye kikosi cha Simba chenye masikani yake mtaa wa Msimbazi Karikaoo ni ule ambao kikosi hiko kilipoteza kwa kufungwa goli 5-1 na Watani wao wa jadi kikosi cha Wanachi.
Vita ya ndani ya uwanja ambayo itanogesha mechi ya Watani wa jadi itakua inawahusu Bacca na Ateba kutokana na aina yao ya uchezaji. Bacca anasifika kwa kukaba kwa nguvu na akili nyingi awapo uwanjani atakabiliana na Mshambuliaji ambaye anauwezo mkubwa wa kutumia nguvu, akili na uwezo mkubwa kufunga akiwa kwenye eneo lolote ndani ya boksi la Mpinzani.
Yanga imeboresha kikosi chao kwa kuongeza Wachezaji wawili waliowahi kukitumikia kikosi cha Simba Clatos Chota Chama na Jean Baleke Otosi, pia Mshambuliaji wa kutoka Azam Prince Dube naye amejiunga na Wananchi baada ya mgogoro wa muda mrefu na timu yake yenye masikani yake Chamazi. Wekundu wa Msimbazi wamewaongeza kikosini Yusuph Kagoma, Lionel Ateba, Debora Fernandez Mavambo, Agustine Okajepha, Lionel Ateba na Abdulrazak Hamza sambamba na Mlinda mlango Moussa Camara.
Mchezo wa mwisho timu hizi mbili kongwe nchini Tanzania zilikutana kwenye mchezo wa ngao ya Jamii kabla ya msimu wa 2024-2025 kuanza ambapo Simba ilifungwa 1-0 na Yanga hivyo inaufanya mchezo wa Oktoba 19, 2024 kutabiriwa utakuwa na ugumu na msisimko mkubwa.