Monday , 14th Oct , 2024

Kila ifikapo Oktoba 14, ya kila mwaka Watanzania wanasherehekea maadhimisho ya kumbukizi ya aliyekuwa mkombozi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambapo baadhi ya wananchi Mkoa wa Dar es Salaam wanaelezea namna uzalendo wa baba wa Taifa ulivyowapa uhuru wa kufanya shug

EATV imefika mtaa wa Butiama kata ya Vingunguti unaobeba jina la mahali alipozaliwa baba wa Taifa, na wao wanaelezea namna uzalendo wa Mwalimu Nyerere ulivyowapa uhuru wa kufanya shughuli za kiuchumi.

“Cha kwanza tunamkumbuka kwa uzalendo wake, cha pili alituunganisha ndio maana akatuweka pamoja visiwani Zanzibar na Tanzania bara Kama unavyoona mimi mtu wa bara lakini leo nipo Vingunguti nafanya shughuli zangu na hii inanisadia mimi kutanua mawazo yangu mahali popote napoishi bila kuhofia au kukutana na ubaguzi wowote “, JOSEPH ABDALLAH-Mkazi wa Butiama Vingunguti.

“Viongozi wengi wa Sasa hivi wamekuwa wakijilimbikizia mimali lakini baba wa Taifa alikuwa mzalendo kaachia madaraka mwenyewe karudi kulima kitu ambacho kwa viongozi wa Sasa hivi ukikuti lakini pia alikuwa anachukia Rushwa kwa watendaji na viongozi wa Serikali kwakweli alikuwa mtu bora sana kwenye Taifa letu ndio maana aliweza kuunganisha mataifa mengine yaliyopata changamoto au migogoro ya kiaisa”, GEORGE MAHEMBE-Mkazi wa Butiama Vingunguti.

“Baba wa Taifa alikuwa kiongozi bora sana sikuwepo wakati anazaliwa lakini mambo mengi mazuri tuliyoyasoma yanamueleza yeye alikuwa ni mtu wa namna gani, tunamuombea sana Mungu ampunguzie adhabu huko aliko tunamuomeba sana”, JOSEPH YOHANA-Mkazi wa Butiama Vingunguti.

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa Rais  wa Kwanza wa Tanzania alizaliwa tarehe 13 Aprili, mwaka 1922 katika kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma katika Mkoa wa Mara, Alikuwa mtoto wa Chifu Nyerere Burito na Bibi Christina Mugaya Wanyang’ombe.

Tarehe 14 Oktoba 1999, ni siku ambayo Taifa la Tanzania halitaisahau kamwe kwani Mwalimu Nyerere aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika Hospitali ya St. Thomas iliyoko jijini London, Uingereza baada ya kuugua kansa ya damu, Mwili wa Mwalimu ulipokelewa jijini Dar es Salaam tarehe 18 Oktoba, 1999 na kupelekwa nyumbani kwake Msasani. 

Tarehe 20 Oktoba, 1999 mwili wa Baba wa Taifa ulipelekwa Uwanja wa Taifa ili Watanzania kwa ujumla waweze kumuaga mpendwa wao, ambapo  21 Oktoba, 1999 ilifanyika sala ya mazishi ya Kitaifa katika uwanja huo ambayo iliongozwa na Muadhama Polycarp Kardinali Pengo, msiba ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi . Watu waliendelea kumuaga Baba wa Taifa Taifa usiku na mchana hadi 22 Oktoba, 1999 jioni mwili wake ulipoondolewa na kusafirishwa kwenda Musoma na hatimaye ukasafirishwa kwenda kijijini kwake Butiama kwa ajili ya mazishi, Mazishi ya Mwalimu Nyerere yalifanyika tarehe 23 Oktoba, 1999 nyumbani kwake huko Mwitongo katika kijiji cha Butiama, wilayani Musoma Vijijini, mkoani Mara.