Sunday , 6th Oct , 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko, ameipongeza Wizara ya Madini kwa mkakati wanaoutekeleza ambao unawazesha upatikanaji wa akiba ya dhahabu  kupitia Benki Kuu ya Tanzania jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko,

Hayo yamesemwa wakati wa ufunguzi wa maonesho ya saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yenye kauli mbiu ya "Matumizi ya teknolojia sahihi ya nishati safi  katika sekta ya Madini kwa maendeleo endelevu" yanayofanyika mkoani Geita. 

"Sisi utajiri ambao Mungu ametujaalia ni utajiri wa madini ikiwemo dhahabu, lazima madini haya yawe chachu katika ukuaji wa uchumi wetu, naipongeza Wizara ya Madini kwa bidii kubwa mliyoifanya sasa ya kuanzisha na kusukuma uwepo wa akiba ya dhahabu kupitia Benki kuu ya Tanzania," amesema Dkt Biteko

Kwa upande wake Waziri wa Madini Anthony Mavunde, ameeleza kwamba kwa sasa baada ya kukaa pamoja baina ya serikali na wadau wamefikia muafaka na hakuna mgomo tena wa kutoiuzia dhahabu BOT baada ya ufafanuzi wa baadhi ya hoja na elimu kutolewa ikiwa ni sehemu ya falsafa ya maridhiano inayohubiriwa kwa nguvu na Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan.

Mavunde ametoa rai kwa wadau wote kushirikiana na serikali katika mpango huo wa upatikanaji wa akiba ya dhahabu kupitia BOT na kuahidi kutoa ushirikiano katika kushughulikia changamoto mbalimbali zitakazojitokeza.