Friday , 27th Sep , 2024

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deus Sangu, amewataka wazazi kutimiza jukumu la malezi ya watoto badala ya kuwaachia walimu peke yao kutokana na wimbi kubwa la mmonyoko wa maadili linaloikumba jamii.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deus Sangu

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu katika mahafali ya 37 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kibakwe wilayani humo.

Amesema kitendo cha jumla ya wanafunzi 80 kuacha shule kati ya wanafunzi 247 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2021 kutokana na sababu za utoro na mimba, hii inaonesha kuwa kuna baadhi ya wazazi hawawajibiki ipasavyo.

"Leo jumla ya watoto 157 wanahitimu kidato cha nne huku tukiwa tumepoteza watoto 80 kutokana na tatizo la utoro na mimba za utotoni, hii sio sawa wazazi liangalieni hili" amesisitiza Mhe.Sangu

Ameongeza kuwa, "Elimu ndio msingi wa kila kitu ukiamua kuwa mfanyabiashara ni lazima uwe na elimu ukitaka kuwa mjasiriamali ni lazima uwe na elimu ndio maana Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anahakikisha watoto wote wanapata elimu bila ubaguzi wowote"  amesisitiza Mhe.Sangu

Kufuatia hatua hiyo Sangu amewataka wazazi kujiepusha na tabia ya kuwaozesha mabinti katika umri mdogo badala yake wahakikishe wanakumbatia elimu itakayowaandaa kwa ajili ya kupambana na maisha

Katika hatua nyingine, Mhe.Sangu amesema Serikali inatarajia kuwapangia vituo vya kazi   jumla ya walimu 247 katika Mkoa wa Dodoma hususan katika wilaya ya Mpwapwa   kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa walimu unaoikumba wilaya hiyo.