Tuesday , 24th Sep , 2024

Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha linachunguza kifo cha Johnson Josephat maarufu kwa jina Sonii (39), mkazi wa Unga Limited Jijini Arusha aliyefariki dunia Septemba, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justine Masejo

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema,"Septemba 23,2024 muda wa saa 11:30 jioni Askari Polisi alifika katika maeneo ya Unga Limited kwa ajili ya kumkamata mtu huyo kuhusiana na tuhuma za kuvunja stoo na kuiba na wakati wa ukamataji alifanikiwa kumvisha pingu mkono mmoja baadaye lilijitokeza kundi la watu na kumshambulia askari kuzuia mtuhumiwa huyo asikamatwe na kufanikiwa kumtorosha kwa kutumia pikipiki,".

Kamanda Masejo amebainisha kuwa taarifa za awali zinaeleza kuwa katika harakati za kumtorosha mtuhumiwa huyo, alianguka na baadaye ndugu walimfikisha hospitalini ambapo alifariki dunia akipatiwa matibabu, "Uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo cha mtu huyo,".