Friday , 20th Sep , 2024

Katiba Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amewataka viongozi wa kamati ya muda ya Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC) kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Amesema Kamati hiyo inatakiwa kuunda kamati itakayosaidia kufanya maboresho ya katiba, kanuni na miongozo mbalimbali itakayosaidia katika usimamizi wa shughuli za kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini.

“Uwepo wa kanuni na miongozo katika mchezo huu ndio nguzo pekee ya kusimamia weledi, kuondoa migogoro na kujenga mahusiano na wadau, kwa ajili ya kuendelea kuinua mchezo huu,”amesema Msitha

Ameongeza kuwa kushirikiana na TPBRC wataandaa mafunzo kwa makocha na mabondia wa ngumi za kulipwa nchini kuwajengea uelewa wa masuala muhimu ya mikataba, bima za afya, kujiunga na mifuko ya jamii na mahusiano mazuri na wadau.

“Kuwepo kwa elimu hizo zitawasaidia mabondia wetu kufanya vizuri katika kazi zao lakini pia katika masuala la afya baada ya kuweza kupata bima ya Afya,” amesema Katibu mtendaji huyo.