Juto Ally katikati akiwa na wajukuu zake wamesimama.
Akiongea na EATV anasema hawajui hatma yao kwani toka Waziri aondoke na kuacha ahadi imeshapita miezi miwili na hakuna mtu yeyote aliyekuja kuwauliza kuhusu changamoto yao.
"Mjukuu wangu tunaishi tu hapa lakini hatujui lini tutatatuliwa changamoto yetu kwa maana toka waziri ania ahidi hajarudi tena na hapa hatujui kama tutapata haki yetu maana wale majamaa hawakawii kuja kutufanyia fujo na sisi maskini hatuna guvu za kupambana nao, namuomba Waziri wa Ardhi aweze kuendelea pale mwenzake alipoishia tuweze kupata haki yetu", alisema Juto Ally, Mmiliki wa Nyumba.
Aidha mjukuu wa mwenye nyumba anaelezea jitihada walizofanya kuhakikisha bibi yao anapata haki yake.
"Baada ya waziri kuondoka tulienda Mahakamani tukaambiwa kesi imerudishwa kwa RPC wa Kinondoni, nikafika ofisi za RPC na yeye akasema bado kwake haijafika, hatujajua hatma yetu kama tutafanikiwa kupata haki yetu au lah, na waziri aliyetuahidi amehamishwa wizara tuna mashaka sana, tuna hofu sana ya kupoteza haki ya bibi yetu", alisema Said Mzee, Mjukuu wa mwenye Nyumba.
"Hapa nilipo nina miaka zaidi ya 50, bibi ana miaka zaidi ya 100 bado ana hangaika na migogoro mwisho wa siku atakufa hajapata haki yake, tnaomba Serikali imsaidie aweze kupata haki yake", alisema Ismail Mussa, Mjukuu wa mwenye Nyumba.
Mgogoro wa nyumba hiyo unamhusu Juto Ally dhidi ya mtu aliyemkopesha hela miaka zaidi ya 15 iliyopita ambaye alikuchukua hati ya nyumba kama dhamana lakini baadae alidai walikubaliana ampe hela na wao watoe hati ya nyumba licha ya mwenye nyumba kulipa kiasi cha fedha alichokopeshwa.