Saturday , 10th Aug , 2024

Tanzania imeahidi kukamilisha mchango wake wa mwaka katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kuzisisitiza nchi nyingine wanachama kufanya hivyo ili kuiwezesha Jumuiya hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba

Hayo yamejiri wakati wa Kikao cha Kamati ya Fedha cha Jumuiya ya SADC kilichofanyika tarehe 10 Agosti 2024, Harare, Zimbabwe.

Katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba ambaye ameambatana na Mratibu wa Kitaifa wa Masuala ya SADC kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha, Bw. James Msina.

Akichangia katika mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba amesema kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa majukumu yanayotekelezwa na Jumuiya kwa ustawi wa kanda hivyo, itaendelea kuwa mwanachama hai na kukamilisha michango yake mapema ili kuwezesha Jumuiya ya SADC kutekeleza vyema shughuli zake, ambazo nchi yetu ni mnufaika.