Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu amesema kuwa serikali katika utekelezaji wa R4 imekamilisha mchakato wa marekebisho ya sheria ya reli ambayo sasa itaondoa ukiritimba na kuruhusu sasa waendeshaji binafsi kutumia reli zilizopo kwa ajili ya kutoa huruma ya usafirishaji
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Ikulu Dar es Salaam, leo tarehe 29 Julai, 2024.
"Niwataarifu pia kwamba tukiongozwa na falsafa ya R4 serikali imekuja na mageuzi ya kuondoa ukiritimba katika uendeshaji wa shughuli za reli, tumerekebisha sheria ya reli ili kuruhusu waendeshaji binafsi kutumia miundombinu hiyo kutoa huduma za usafirishaji, kanuni zipo tayari hivyo ndugu zangu naomba mchangamkie hiyo fursa"
Aidha Rais Samia amesema Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika ukuaji wa uchumi licha ya Changamoto zinazoikumba dunia kwa sasa
"Pamoja na changamoto mbalimbali tunazoshuhudia kwenye uchumi wa dunia, uchumi wetu umekuwa himilivu na umeendelea kukua na kuimarika zaidi, mwaka 2023 uchumi wetu ulikuwa kwa asilimia 5.2 ukilinganisha na asilimia 4.7 mwaka 2022 na mfumuko wa bei umeendelea kubaki asilimia 3 ndani ya lengo letu"
Kuhusu umeme wa uhakika Tanzania Rais Samia amesema maemdeleo ni mazuri kutokana na kuanza kuwashwa kwa vinu katika bwawa la mwalimu Nyerere
"Kwa upande wa changamoto ya nishati ya umeme kwa sasa kama mnavyoelewa bwawa letu la Mwalimu Nyerere limeanza kuzalisha umeme mashine tatu tayari tumeshawasha tuna umeme wa ziada wa megawati 705 ambao tayari umeingia kwenye Grid ya taifa"
"Pamoja na mafanikio haya tunatambua kuwa bado tuna kazi ya kufanya hasa kwenye njia za upokeaji na usafirishaji wa umeme kwenye maeneo kadhaa ya Tanzania kazi ambayo tunajipanga iendelee vizuri"