Tuesday , 9th Jul , 2024

Aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Yahaya Nawanda, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza na kusomewa shitaka moja la kumwingilia kinyume na maumbile Tumsiime Ngemela (21) katika eneo la Rock City Mall jijini Mwanza.

Aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Yahaya Nawanda

Mshtakiwa huyo amefikishwa katika mahakama hiyo mapema leo Julai 9, 2024 na kusomewa shitaka hilo ambalo anadaiwa kulitenda Juni 2, 2024 katika eneo hilo kinyume na kifungu cha sheria cha 154 kifungu kidogo (a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022

Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Erick Maley, Waendesha mashtaka wa kesi hiyo ambao ni Wakili wa serikali Magreth Mwaseba na Martha Mtiti waliitaja kesi hiyo kuwa ni kesi namba 1883 ya mwaka 2024.

Hatahivyo mshtakiwa alikana shtaka hilo na yuko nje ya dhamana baada ya kukamilisha masharti aliyokuwa amewekewa ambayo ni kuwa mtumishi wa serikali pamoja na bondi  ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh 5 milioni.

Baada ya kukamilisha masharti hayo, Mshtakiwa yupo nje ya dhamana hadi Julai 16, 2024 ambapo kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa hoja za awali huku upande wa mlalamikaji ukitakiwa kwenda na mashahidi.