Monday , 8th Jul , 2024

Sherehe ya kuwasimika Rika la watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 17 la kabila la Kimaasai imefanyika huku jamii hiyo ikitakiwa kujiweka kando na tamaduni zisizofaa.

Sherehe hizo zimefanyika katika eneo la Mandila, katika Kijiji cha Mserekia, Mabogini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo Irmegoliki wapatao 100 wamesimikwa huku Nuru Taiko-Maningo, na Msaidizi wake Papa Letaolo wakiteuliwa kusimamia kundi hilo.

Akizungumza baada ya tukio hilo ambalo hufanyika katika zizi la ng'ombe ambalo mlezi wa Rika hilo hupewa watoto hao, Chifu Noel Jumbe Makeseni wa Moshi amesema kutokana na mmomonyoko wa maadili jamii ya Kimaasai ya Mserekia inaendelea na juhudi mahsusi za kuhakikisha utamaduni wao haupotei.

Aidha kiongozi wa Kimila Leigwani Kiroiya Taiko ameweka bayana kuwa kwa sasa wanaendelea kuimarisha uelewa kwa kuwapeleka watoto Shule.

Kwa upande wake mshauri wa Irmegoliki amesema ni furaha iliyoje kuwasimika watoto wa rika hilo kwa madhumuni ya kuimarisha maadili Bora kwa jamii ya Kimasai kuanzia utotoni.

Awali sherehe hizo zilianza kwa Irmegoliki kuwekwa wakfu wa kunyunyiziwa Maji na kupakwa asali iliyochanganywa na kinyesi cha ng'ombe dume pamoja na mafuta ya kidali cha ng'ombe ikiwa ni ishara ya kuwatakia amani, Upendo, mshikamano, heshima na utajiri kwa rika hilo.