Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Amesema kuwa mifumo hiyo pamoja na mambo mengine itasaidia kuwabana watumishi wazembe. “Kunahitajika msukumo kuhakikisha mifumo hii inatumika niwaelekeze watendaji wakuu na watumishi wa umma kuhakikisha mnaandaa mipango na mikakati ya muda mfupi na mrefu ya jinsi mifumo ya kidigitali itakavyotumika kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa umma,"
Amesema hayo leo Jumapili, Juni 23, 2024, alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma, ambapo pia alizindua Mifumo ya Kidijitali ya Uwajibikaji na Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma iliyosanifiwa na kujengwa na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora.
Mifumo iliyozinduliwa ni Mfumo Jumuishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (e-WATUMISHI), Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi (PEPMIS kwa watumishi wa umma na PIPMIS kwa taasisi za umma), Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HR Assessment) na Mfumo wa e-Mrejesho.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaelekeza watendaji wakuu na watumishi wa umma waandae mipango inayopimika. “Mipango hii inapaswa kuwa wazi, yenye malengo yanayopimika na kuzingatia mahitaji ya wananchi na matakwa ya sera za Serikali.”