Wednesday , 12th Jun , 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema mikopo ni moja ya vyanzo vya mapato ya serikali kote duniani, hivyo Tanzania kukopa siyo aibu wala kujidhalilisha, bali ni sifa njema kwa kuwa inakopesheka.

Mhe. George Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Simbachawene ametoa kauli wakati akizungumza kwenye harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya kubadilisha paa la Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu,Yuda Tadei  Mang'ola Chini, Wilaya ya Karatu, Mkoani Arusha, ambalo limekuwa likivuja wakati wa mvua  na hivyo kusababisha wakristo kushindwa kukaa ndani.

Amesema vyanzo vya mapato vya Kanisa  ni pamoja na sadaka ya kila jumapili, zaka, misaada mbalimbali pamoja na harambee  huku akitaja   vyanzo vya mapato vya Serikali kuwa  ni kodi, tozo, misaada na mkopo, na kusema  kukopa ni moja ya chanzo cha mapato ya serikali na serikali zote duniani zinakopa.

Aidha amesema kama ingetokea Tanzania haiwezi kukopesheka hiyo ndo ingekuwa  aibu lakini kwa kuwa inakopsheka hiyo ni heshima kubwa kwa watanzania kwa kuwa inakopa ili kutekeleza miradi ya maendeleo  na kama isipofanya hivyo itapelekea  nchi kupata madhara makubwa ambayo yasingetokea kama ingekopa.

Amesema Nchi zote duniani ikiwemo Marekani na China  zinakopa na  zinadaiwa na kwamba kodi inayokusanywa nchini haina uwezo wa kutekeleza miradi hiyo na kama kodi hiyo itaweza kutumika inaweza kuchukua zaidi ya miaka 40 ili kukamilisha miradi hiyo.

"Vyanzo vya mapato vya Kanisa  ni sadaka ya kila jumapili, zaka, misaada mbalimbali pamoja na harambee ambapo harambee ni hatua  ya mwisho ya utafutaji wa fedha kwa Taasisi za dini, lakini vyanzo vya mapato vya Serikali  ni kodi, tozo, misaada na mkopo, hivyo kukopa ni moja ya chanzo cha mapato ya serikali na serikali zote duniani zinakopa"amesema Simbachawene na kuongeza kuwa

"Kukopa  ni chanzo cha mapato hivyo isionekane Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inapokwenda kutafuta mkopo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo  ndo inakopa sana".

Amesema kutokana na mahitaji makubwa ya nchi suala la kukopa haliepukiki akitolea mfano uendelezaji wa Bwawa la kuzalisha  umeme la Mwalimu Julius Nyerere ambalo gharama yake ni zaidi ya  trioni 6 huku bajeti ya Serikali  ya mwaka mzima ikiwa ni tirioni 43 huku zaidi ya asilimia 7O ya fedha hizo zikitumika kwa ajili ya uendeshaji wa nchi na asilimia 30 ndizo hupelekwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo 

" Hivi tungetaka kujenga reli ya SGR kwa kodi yetu  tungejenga kwa miaka mingapi?amehoji  Simbachawene na kusema  ikijengwa kwa miaka 100  itakuwa na tija kweli na tukiamua tutaweza  kujenga kwa miaka 50 au 60 ambapo hapo  tutaacha kulipana mishahara, kusomesha watoto pamoja na kutibu  wagonjwa "

Amesema "Mbali na utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati, Serikali chini Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea na ujenzi wa madarasa ambayo ili kumaliza upungufu wa madarasa uliopo sasa kama zisipokopwa  changamoto hiyo itatuliwa ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka  25 ijayo huku idadi ya watu ikizidi kuongezeka".

"Unataka Rais Samia akae tu asiende kukopa"  amehoji Simbachawene na kususitiza kuwa,

"Kukopa ni chanzo cha mapato  na  kukopa sio kujidhalilisha, Tanzania ina  sifa hiyo  ya kukopa. Nchi inayoweza kukopesheka ni nchi yenye heshima  kama ilivyo Tanzania  kwani mashirika makubwa ya fedha duniani ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la fedha Duniani ( IMF) zimeweka vigezo za vya kuweza kukopesheka na  Tanzania inakopesheka kwa sababu ina vigezo".

Hata hivyo Mhe.Simbachawene amesema kwa mujibu wa kanuni za fedha duniani zinaipa Tanzania wigo wa ukomo wa kukopa na kama nchi bado ina sifa ya kukopa kwa sababu bado haijafikia kikomo hicho.

Amesema "Hivi reli ikishajengwa inarudia tena kujengwa , umeme ukianza kuzalishwa tunarudia tena, viwanja vya ndege, madaraja, madarasa na vituo vya afya vinavyojengwa nchi nzima havirudiwi tena kujengwa na hivi ndo vinajenga uchumi kisha tunasonga mbele" amesema Simbachawene 

"Fedha hizi zinazokopwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi huku akitolea mfano Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Dodoma  ndani ya kipindi cha miaka mitatu chini ya Uongozi wa Rais  Samia Suluhu Hassan  haikuwahi kupata fedha nyingi za maendeleo ndani ya kipindi cha miaka 20 iliyopita".