Thursday , 22nd Feb , 2024

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata kuratibu na kusimamia uchaguzi mdogo wa madiwani kata 23 kwa ufanisi na weledi kwa kuzingatia ratiba ya utekelezaji ili kufanikisha uchaguzi utakaofanyika Machi 20, 2024.

Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Asina Omari akifunga mafunzo kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 23

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Asina Omari wakati akifunga mafunzo kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 23, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Alisema majukumu yaliyo mbele yao ni makubwa na muhimu na yanahitaji umakini, kujitoa na hasa baada ya kupatiwa mafunzo hayo, hivyo aliwasisitiza umuhimu wa kutenga sehemu ya muda wao kusoma Katiba, Sheria na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume ili yawaongoze katika kusimamia uchaguzi utakaokuwa huru na wa haki. 

“Mkikutana na changamoto zozote msisite kufanya mawasiliano na watendaji wa Tume au hata kubadilishana uzoefu kwa kuwasiliana nyinyi kwa nyinyi” alisema Mhe. Jaji Asina.

Alieleza matumaini ya Tume kuwa watateua na kuajiri watendaji wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi za uchaguzi kwani jambo hilo limekuwa likisisitizwa tangu siku ya kwanza ya mafunzo kwa kuwa hao ndio watakaosimamia zoezi la kupiga kura na kuhesabu kura vituoni, kazi ambayo inahitaji umahiri, umakini na weledi katika kutekeleza.

“Ni matumaini na imani iliyonayo Tume kuwa, wakati wa kipindi cha mafunzo ya watendaji wa vituo, mtayafanya na kuyasimamia kwa ufanisi na weledi kwa kuzingatia tarehe zilizopangwa kwenye ratiba ya utekelezaji wa shughuli za uchaguzi.”, alisema Mhe. Jaji Asina.

Alifafanua kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wasimamizi wa vituo ili waweze kufahamu majukumu yao na kuyatekeleza ipasavyo wakati wa uchaguzi, hivyo aliwataka wakamilishe mambo yote muhimu yanayotakiwa kwenye mchakato wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kubandika matangazo na mabango mbalimbali ya kisheria kuhusiana na uchaguzi kwa mujibu wa maelekezo. 

“Wapo wadau mbalimbali wa uchaguzi kama vile vyama vya siasa,wananchi na watazamaji ambao wanafuatilia uendeshwaji wa uchaguzi na kiwango cha uzingatiwaji wa sheria zinazohusiana na uchaguzi. Hivyo, tutekeleze kila hatua na kila jambo linalotakiwa kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi huu.”, alisisitiza Mhe. Jaji Asina.