Wednesday , 21st Feb , 2024

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Juma Mkomi amewataka Maafisa Rasilimaliwatu wote serikalini kuhakikisha wanaweka kumbukumbu sahihi za watumishi wa umma wanaotarajia kustaafu kabla ya miezi sita ili kuwaondolea usumbufu wa kufuatilia mafao yao pindi wanapostaafu.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Juma Mkomi

Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma  wakati akizungumza  kwenye kikao kazi na  watumishi  wa Ofisi yake,   ikiwa ni mwendelezo wa kuhimiza utendaji na  uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini.

"Mtumishi anapewa barua ya kumtaarifu kustaafu kabla ya miezi sita halafu baadaye anaanza kusumbuliwa eti michango ya mafao haionekani, sasa hiyo barua aliyopewa kabla ya miezi sita ilikuwa na maana gani," amehoji Bw. Mkomi.

Amesisitiza kuwa suala hili lazima lifanyiwe kazi kwa kuwa watumishi hao wanaostaafu wamelitumikia taifa kwa moyo hivyo kuhangaishwa sio haki.

Katika hatua nyingine, Mkomi ametoa onyo kwa watumishi wanaovujisha siri za serikali ambapo ameahidi wale wote watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.