Tuesday , 20th Feb , 2024

Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia zimesaini mkataba wenye thamani ya Euro milioni 361.1 sawa na takribani shilingi bilioni 988.093 kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa kuendeleza miundombinu Dar es Salaam {Dar es Salaam Metropolitan Development Project Phase II (DMDP II)}

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete.

Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika jijini Dar es Salam kati ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema DMDP II itaendelea kuboresha miundombinu muhimu ya umma katika wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni zilizokuwepo kwenye awamu ya I ya mradi huo, sambamba na kupanua wigo wa uboreshaji miundombinu katika wilaya zinazoingia katika mradi kwa mara ya kwanza za Ubungo na Kigamboni.

Amesema lengo la mradi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020 -2025 na ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayolenga kutanua na kuboresha miundombinu na huduma katika Jiji la Dar-es-Salaam.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete alisema Benki hiyo inajivunia kuwa sehemu ya ukuaji wa Dar es Salaam ambapo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, benki hiyo imetenga dola bilioni 1.5 kwa ajili ya ufadhili maendeleo ya jiji hilo.