Tuesday , 6th Feb , 2024

Zaidi ya wananchi 63 wilayani Nachingwea mkoani Lindi wamekosa makazi kufuatia mvua kubwa iliyonyesha wilayani humo na kuharibu nyumba zao huku zingine zikiachwa na nyufa za kuogofya.

Wakizungumza na #EastAfricaTV wananchi hao wameiomba serikali iwasaidie wapate hifadhi salama huku walio katika mazingira ya hatari wakitakiwa kuhama mara moja kwani mvua hazijatabirika mwisho wake na muda wowote wanaweza kudondokewa na nyumba mbovu zilizokosa msingi.

Kutokana na mvua kubwa kunyesha, wananchi hawa ambao kwasasa hawana makazi, wameioomba serikali iangalie namna ya kuwasaidia kwani wengine wanaishi kwa marafiki zao na majirani huku wengine wakijitoa kafara kwa kulala kwenye nyumba zilizoharibika kwa kuegesha miti, jambo linalotajwa kuwa ni la hatari zaidi kwani muda wowote nyumba hizo zinaweza kudondoka.

"Kwa sasa mimi naishi kwa rafiki zangu baada ya ukuta wa nyumba yangu kutitia, naiomba serikali itusaidie kwa sababu kwa sasa hatuna chochote," amesema mmoja wa wananchi hao.

Akifanya tathmini na kuangalia athari iliyotokana na mvua hiyo kubwa, Mkuu wa wilaya ya Nachingwe Mohammed Moyo, ametembelea eneo la tukio na kuwapa pole waathirika wa mvua hiyo, huku akisisitiza tahadhari zaidi kwa wakazi wa eneo hilo wasitumie nyumba zao zilizokwishabomoka kwani muda wowote zinaweza kuwadondokea.