Friday , 15th Dec , 2023

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema eneo la ununuzi wa umma limekuwa likiripotiwa kugubikwa na vitendo vya rushwa na ubadhirifu ambapo zaidi ya asilimia 72 ya bajeti ya Serikali imekuwa ikitumika kwenye manunuzi  hayo.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete

Amesema kutokana na  uzito huo serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao imeamua kusanifu, kujenga na kusanikisha Mfumo wa Kitaifa wa Kielektroniki wa Ununuzi Tanzania {National e-Procurement System of Tanzania (NeST)} ili kuweza kukabiliana na changamoto hiyo. 

Ametoa kauli hiyo leo Jijini Arusha wakati akifunga kongamano  la 14 la mwaka la wataalam wa ununuzi na ugavi zaidi ya 900 lenye kauli mbiu "Mabadiliko ya kidijitali kwa ajili ya kuboresha usimamizi na ugavi kelekea maendeleo endelevu"

Amesema mfumo huo utasaidia  kuondoa mianya ya rushwa na upendeleo na hivyo thamani ya pesa za Serikali katika bidhaa na huduma italindwa kwani kutakuwa hakuna  ulazima wa  watu kukutana ana kwa ana

"Ni furaha yangu mimi kama Naibu Waziri ninayeshughulikia Utawala Bora ambapo ninasimamia uzuiaji na mapambano dhidi ya rushwa, naamini mfumo huu utaondoa hisia hasi zilizojengeka katika jamii kwenye suala la manunuzi ya umma na hivyo kuongeza uwazi," amesema Mhe.Kikwete 

Mhe.Kikwete amesema mfumo huo utaongeza ufanisi, uwazi na ushindani katika ununuzi wa umma. 

Katika hatua nyingine, Mhe.Kikwete amesema serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayesababisha upotevu wa rasilimali za nchi huku akiwataka wasithubutu kucheza na mfumo huo mpya wa manunuzi kwa umma.