Thursday , 23rd Nov , 2023

Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imeahidi kutoa milioni 20 ili kuimarisha kivuko cha Magole na Mwanagati kilichopo katika Kata ya Mzinga Halmashauri ya Ilala mkoani Dar es Salaam ili kuweza kupitika muda wote.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama, wakati akizungumza na wakazi waliojitokeza katika eneo hilo la kivuko liloathirika na mvua wakati wa ziara yake iliyolenga kupata taarifa zilizochukuliwa na kamati ya mkoa ya maafa juu ya kudhibiti madhara zaidi ya mvua yanayoweza kujitokeza.

Ameongeza kusema kazi ya kuimarisha kivuko ifanywe na wakala wa barabara vijijini TARURA haraka iwezekanavyo.

Waziri Mhagama amesema kuwa serikali inatamani kuona shughuli za wananchi zifanyika bila kusimama, "Tunatamani watoto wetu waende shule, tunatamani kina mama wajawazito waende kupata huduma za afya kwa wakati, tunapenda wananchi wajisikie serikali yao inawajali,"

Waziri Mhagama alielekeza TARURA kuifanya kazi hiyo  kwa uaminifu mkubwa na kwa hofu ya Mungu, kwa sababu wanasimamia uhai na maisha ya watu na serikali imewaamini na inawategemea