Saturday , 18th Nov , 2023

Rais wa Liberia George Weah amempigia simu mpinzani wake katika kinyang'anyiro cha urais, Joseph Boakai, kumpongeza kwa ushindi wake.

Katika hotuba yake kwa taifa alisema "watu wa Liberia wamezungumza na tumesikia sauti yao".Mgombea wa upinzani anaongoza kwa kura 28,000 huku karibu kura zote zikihesabiwa.

Nyota wa zamani wa mpira wa miguu, Rais Weah amekuwa madarakani tangu 2018. Atajiuzulu mwezi Januari.Aliingia kazini kwa wimbi la shauku, hasa kutoka kwa wapiga kura vijana, baada ya kushinda uchaguzi huo  pia dhidi ya Bw Boakai  kwa kiwango kikubwa.

Lakini mtazamo kwamba alishindwa kukabiliana na ufisadi, kupanda kwa bei na kuendelea kwa matatizo ya kiuchumi kulichafua taswira yake.

Duru ya pili kati ya Bw Boakai na Bw Weah ilichochewa baada ya kukosekana mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika duru ya kwanza ya mwezi uliopita. Kulikuwa na wagombea wengine 18.