Monday , 6th Nov , 2023

Kiongozi wa chama cha ACT wazalendo Zitto Kabwe amesema licha ya Chama hicho kushinda kiti cha Ubunge katika  Uchaguzi mdogo wa jimbo la Mtambwe mjini unguja visiwani Zanzibar bado kuna jitihada za makusudi zinahitajika kufanyika ili kuhakikisha Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 unakuwa Huru

Ameyasema hayo Mjini Unguja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema katika uchaguzi huo chama hicho kimeshuhudia matukio mengi yasiyo yakiungwana na yenye kukiuka utawala wa sheria jambo linalohatarisha amani na kama mambo hayo yakiendelea mwaka 2025 kutashuhudiwa uchaguzi mbaya zaidi kuliko wa mwaka 2020.

"Tumeona tuzungumze na wananchi kupitia ninyi wana habari, ili kuonyesha Dunia na kuwaonyesha wananchi uhuni mkubwa ambao Chama cha Mapinduzi na Serikali yake  pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama,wamefanya na vinatutia wasiwasi kwamba mambo haya yakiendelea mwaka 2025 tutakuwa na Uchaguzi mbaya zaidi kuliko hata wa mwaka 2020 , kwa maana ya Vurugu, Mauwaji na watu kuumia, jambo ambalo tusingependa kuliona sisi kwa upande wetu ACT-Wazalendo"

''Tunapenda kuyaeleza haya kwasababu tumeshuhudia Vitimbi na hujuma za wazi katika Uchaguzi ule mdogo kule mtambwe, licha ya kwamba tupo katika Serikali ya umoja wa Kitaifa na kufuatia kuwepo kwetu kwenye Serikali ya umoja wa kitaifa hali ya utulivu imekuwa ni kubwa  hapa Zanzibar lakini ni kama Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na vyombo vyake na Chama cha Mapinduzi hawajali kutonesha vidonda  ambavyo tulitarajia viwe vimeanza kukauka lakini kila chaguzi ndogo inapotokea vidonda vile vinatoneshwa na inaonyesha matarajio ambayo tunakuwa nayo kuelekea 2025 ni matarajio Hewa"- Zitto Kabwe Mwenyekiti ACT Wazalendo