Wednesday , 18th Oct , 2023

Mahakama ya wilaya ya Njombe imemhukumu Joseph Msemwa (27), Mbena na mkazi wa Njombe, kutumikia jela kifungo cha miaka 180 jela kwa makosa sita ya ulawiti na ubakaji ambapo kila kosa limekuwa na hukumu ya miaka 30.

Joseph Msema

Kijana Joseph Msema anadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti, baada ya kuwahadaa wanawake watatu na kisha kuwafungia katika nyumba aliyokuwa anaishi katika mtaa wa Kihesa, na kisha kuwalawiti na kuwabaka kwa zamu usiku na mchana, zoezi lililoenda sambamba na kuwaingiza magunzi ya mahindi na matango katika sehemu za siri.

Akisoma hukumu ya kesi hiyo nambari 53 ya mwaka 2023, Hakimu Mkazi wa wilaya ya Njombe Matilda Kayombo, amesema mshtakiwa Joseph amekutwa na hatia katika makosa sita, matatu yakiwa ni ubakaji na matatu ya ulawiti anayodaiwa kuyafanya siku ya tarehe 16 hadi 23 mwezi Mei mwaka 2023 katika mtaa wa Kihesa Kilimani, mkoani Njombe.

Matilda ameendelea kusema Mahakama imemtia hatiani baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na mashahidi saba, wakiwemo waathirika wa matukio, taarifa ya uchunguzi wa daktari, uongozi wa serikali ya mtaa pamoja na polisi.

Taarifa zilizosaidia kukamatwa kwake zinaelezwa na mahakama kuwa zilitolewa na mmoja kati ya wanawake aliokuwa amewateka, ambae alifanikiwa kutoroka na kupiga ndulu kwa majirani ambao walivamia nyumbani kwa Joseph na kukuta wanawake wengine wawili wakiwa ndani, vile vile kulikutwa mfuko ukiwa na dawa za kienyeji, huku mahakama ikieleza kuwa sehemu ya ushahidi uliotolewa ulibainisha kuwa mtuhumiwa baada ya kuhojiwa alikiri kwamba alifanya matukio hayo akiwa anatekeleza maagizo ya mganga aliyemtaka abake wanawake na watoto.

Waendesha mashtaka wakiongozwa na Magdalena Whelo na Elise James waliiomba mahakama kutoa hukumu kali kwa mtuhumiwa ili iwe funzo kwa jamii yote ikizingatiwa kwamba matukio ya ubakajai na ulawiti yamekuwa yakiongezeka maradufu Njombe.