
Israel leo imeonya raia wasiwe ndani ya takriban kilomita 4 (maili 2.5) kutoka mpaka wa Lebanon la sivyo wanaweza kupigwa risasi. Imewaambia watu wanaoishi katika maeneo ya mpaka ambayo yamejaa miji midogo na vijiji kukaa karibu na makazi.
Haya yanajiri baada ya mtu mmoja kuuawa katika mashambulizi ya Hezbollah Jumapili asubuhi, ambayo yalikabiliwa na mizinga kutoka upande wa Israel. Hezbollah imesema mashambulizi yake yalikuja kujibu mashambulizi ya Israel nchini Lebanon siku moja kabla ambayo yaliwaua raia wawili na mpigapicha wa Shirika la habari la Reuters ambaye alikuwa akipiga picha karibu na mpaka.
Hatua ya Israel siku ya Jumapili inaashiria hatua kubwa katika juhudi za kujiandaa kwa uwezekano kwamba Hezbollah huenda ikafungua mkondo wa pili na kuja kuwasaidia wapiganaji wa Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Israel pia imevishambulia viwanja vya ndege vya Aleppo na Damascus nchini Syria katika juhudi za kuzuia Iran kutumia Syria kuingia katika mzozo huo. Tehran haijatishia rasmi kujiunga na vita hivyo lakini imesema Israel itakabiliwa na madhara iwapo haitasitisha mashambulizi yake dhidi ya Gaza.