Wednesday , 11th Oct , 2023

Watendaji wa Vijiji na Kata Mkoani Shinyanga wameonywa kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuwaozesha wanafunzia kwa kushirikiana na wazazi  watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akizungumza na watendaji wa Vijiji, Kata na maafisa Tarafa kutoka Halmashauri tatu za Mkoa huo ambao hawaonekani pichani.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme wakati akizungumza na watendaji wa Vijiji,Kata na maafisa Tarafa kutoka Halmashauri tatu za Mkoa huo ambapo amesema wapo baadhi ya watendaji wanajihusisha na rushwa.

Mkuu wa Mkoa amesikitishwa na kitendo cha mwanafunzi kuozeshwa wakati kuna viongozi kuanzia ngazi za Vitongoji,Vijiji na Kata lakini hawatowi taarifa na kuwataka kuacha kupokea hongo ili wafumbie macho matukio hayo.

“Inasikitisha mwanafunzi anaolewa na sherehe inafanyika na nyinyi baadhi yenu mnahudhuria wakati mkijua kabisa ni mwanafunzi hamchukuwi hatua,acheni tabia hiyo fanyeni kazi yenu tukomeshe matukio haya”amesema

Mpaka  sasa wanafunzi watatu wamenusurika kuozeshwa na wazazi wao katika Halmashauri ya Shinyanga,Kishapu na Manispaa ya Shinyanga akiwemo mwanafunzi wa kidato cha tano ambaye ndoa yake ilivunjwa baada ya kupata taarifa za siri.

Kufuatia maagizo hayo baadhi ya watendaji wa Kata na Vijiji wamesema wanakwenda kusimamia maagizo yaliyotolewa na serikali ikiwemo kuzuia wanafunzi kuozeshwa na kuchukuwa hatua kwa wazazi watakao bainika.

Budugu Kasuka Mtendaji wa Kata ya Nyamalogo amesema kitendo cha kupokea hongo na kuruhusu kuozesha wanafunzi kinakiuka haki za msingi za mtoto kupata elimu na kueleza kuwa kama kuna watendaji wanafanya vitendo hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Mtendaji wa Kata ya Salawe Emmanuel Maduhu amesema wanakwenda kusimamia Miradi ya maendeleo ili ilete tija kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kufichuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto ili kukomesha matukio hayo.