Monday , 9th Oct , 2023

Mapambano kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas yameendelea hadi siku ya Jumatatu katika miji ya kusini mwa Israel.

Idadi ya vifo na majeruhi inazidi kuongezeka huku maelfu ya watu wakilazimika pia kuyahama makaazi yao. 

Mapigano yanaendelea kwa siku ya tatu mfululizo kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hamas. Msemaji wa jeshi la Israel, Richard Hecht, amesema bado wanapambana katika angalau maeneo saba yaliyopo kusini karibu na eneo la pwani, lakini taarifa za sasa zinasema jeshi la Israel inasema wamechukua udhibiti wa maeneo yaliyoshambuliwa na Hamas.

Serikali ya Tel Aviv imewatuma makumi ya maelfu ya wanajeshi katika Ukanda wa Gaza na imeapa kulishinda kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina.

Jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga mara tu baada ya kundi la Hamas kuivamia Israel kwa kushtukiza siku ya Jumamosi kwa kurusha maelfu ya makombora huku mamia ya wapiganaji wakiingia hadi Israel na kufanya mauaji.

Israel imeshtushwa na shambulio hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa katika eneo lake. Hadi sasa zaidi ya watu 700 wameuawa Israel huku 430 wakiuliwa huko Gaza. Mwishoni mwa juma, Hamas waliwauwa takriban watu 250 waliokuwa wakihudhuria tamasha la muziki karibu na Gaza.

Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Galant ameamuru "kuzingirwa kamili" kwa Gaza, akisema mamlaka itakata umeme na kuzuia kuingia kwa chakula na mafuta eneo hilo. Israel na Misri zimeiweka vikwazo mbalimbali Gaza tangu Hamas iliposhinda uchaguzi na kuchukua madaraka kutoka kwa watawala wa Palestina mnamo mwaka 2007.