Wednesday , 13th Sep , 2023

Serikali imewataka wananchi kuepuka kuingiza nchini na kutumia majokofu au viyoyozi vilivyokwishatumika (mtumba) ambavyo vinatumia gesi haribifu kwa tabaka la ozoni na badala yake watumie bidhaa zenye uwezo mdogo wa kuchangia ongezeko la joto duniani.

Waziri wa Nchi Ofisi Ya Makamu Wa Rais (Muungano Na Mazingira) Mhe. Dkt.Selemani Jafo

Waziri wa Nchi Ofisi Ya Makamu Wa Rais (Muungano Na Mazingira) Mhe. Dkt.Selemani Jafo, amesema hayo wakati akitoa tamko kuhusu Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni jijini Dodoma leo Septemba 13, 2023.

Amesema hayo wakati Tanzania ikitarajia kuadhimisha siku hiyo ifikapo Septemba 16, 2023, kama kumbukumbu ya tarehe ya kutiwa saini Itifaki ya Montreal ya mwaka 1987 kuhusu kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni ambalo kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya mionzi ya jua isifike kwenye uso wa dunia.

Dkt. Jafo amesema tabaka la ozoni linapoharibiwa husababisha saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi, kujikunja kwa ngozi, kuathirika kwa ukuaji wa mimea pamoja na kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo, alitoa wito kwa wananchi kununua bidhaa zilizowekwa nembo rasmi isemayo "Ozone friendly" au "low global warming potential".

Madhara mengine aliyataja kuwa ni kuathirika kwa ukuaji wa mimea vile vile,baadhi ya kemikali hizi husababisha kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi.