Thursday , 31st Aug , 2023

China imeiambia India "kukaa kimya" juu ya ramani mpya ya China ambayo Delhi inasema inadai eneo lake.India iliandamana baada ya Beijing kutoa ramani inayoonyesha jimbo la kaskazini mashariki la Arunachal Pradesh na eneo linalozozaniwa la Aksai Chin kama eneo la China.

Beijing ilijibu kwa kusema majirani zake wanapaswa kujiepusha na "kutafsiri zaidi" suala hilo.

Wakati huo huo, ripoti za vyombo vya habari zinasema Rais Xi Jinping wa China huenda asifanye mazungumzo ya viongozi wa G20 wiki ijayo mjini Delhi.

Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinaashiria kuwa waziri mkuu Li Quang atahudhuria mkutano huo. Bwana Xi awali alithibitisha kuwa atasafiri kwenda Delhi kwa mkutano huo kuanzia Septemba 9-10 - lakini wizara ya mambo ya nje ya China haitathibitisha kuhudhuria kwake alipotakiwa kufanya hivyo katika mkutano wa kawaida na waandishi wa habari siku ya Alhamisi.

India sio nchi pekee inayopinga ramani hiyo ,siku ya Alhamisi, Ufilipino na Malaysia zilitoa maandamano dhidi ya madai ya China ya umiliki wa sehemu kubwa ya bahari ya kusini mwa China katika ramani. Taiwan  ambayo China inasema ni jimbo lililojitenga ambalo hatimaye litakuwa chini ya udhibiti wa Beijing  pia ilipinga kuingizwa kwake katika ramani.