Wednesday , 30th Aug , 2023

Klabu ya Lipuli FC ya mjini Iringa inayoshiriki ligi daraja la pil inatarajiwa kurudi ligi daraja la kwanza baada ya wadau wa soka wa mkoani Iringa (hawakutajwa) kuinunua klabu ya Ruvu Shootings ya daraja la kwanza katika mpango unaolenga kuibadili jina ili itambulike kama Lipuli FC.

Mchakato huo utaifanya pia timu ya African Wanderers ya mjini Iringa inayoshiriki ligi daraja la nne ngazi ya wilaya kupanda hadi daraja la pili baada ya kukamilisha mchakato wa kuchukua nafasi ya Lipuli FC.

Akizungumza na wanahabari mjini Iringa leo, mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada alisema; “Utaratibu wa kuinunua Ruvu Shootings tayari umekamilika na wakati wowote kuanzia sasa timu hiyo itakuja Iringa.”

Bila kutaja thamani ya dili hilo, Ngwada alisema taratibu zingine za kubadili jina la klabu hiyo ili ijulikane kama Lipuli FC zinaendelea.

Kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego, Mstahiki Meya aliwashukuru wadau wote waliotoa fedha zao na kufanikisha mpango wa kuinunua timu hiyo.

“Baada ya kushauriana na baadhi ya wadau wakiwemo viongozi wa mpira mkoani hapa, tumekubaliana Ruvu Shootings ibadilishwe jina na kuitwa Lipuli FC ambayo historia yake ya mpira mkoani hapa inabebwa katika maeneo mengi,” amesema

“Na nafasi ya Lipuli katika ligi daraja la pili tumekubaliana ichukuliwe na klabu yetu ya siku nyingi ya mjini Iringa ya African Wanderers,” amesema

Mdau wa michezo wa mjini Iringa, Eliud Mvella aliwaomba wadau wakiwemo wafanyabiashara wa mkoani hapa kujitokeza kuzisaidia timu hizo kwasababu zitachochea mzunguko wa fedha na uchumi wa Iringa.

Mwenyekiti wa Lipuli FC, Ramadhani Mahano amesema  wataendelea na wachezaji wote wa Ruvu Shootings na wale wa Lipuli walionao sasa watawabakisha kwa African Wanderers.

Hata hivyo baadhi ya wadau wameshauri badala ya timu hiyo ya Ruvu Shootings kuitwa jina la Lipuli, litafutwe jina lingine litakaloifanya timu hiyo iwe na sura ya wana Iringa bila kujali tofauti zao.