Monday , 21st Aug , 2023

Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Frederick Shoo amesema ieleweke kuwa Kanisa linaunga mkono uwekezaji ,  hawapingi uwekezaji na kwamba wanaifahamu nia ya Rais ya kuhusu uwekezaji.

Dkt. Shoo ameyasema hayo leo Agosti 21, 2023 wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la KKKT yaliyofanyika jijini Arusha katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumila ambapo mgeni rasmi alikuwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Naomba ieleweke wazi Kanisa linaunga mkono uwekezaji, hatupingi uwekezaji na tunajua wewe kwenye nia yako unataka uwekezaji, hata hivyo jambo hilo limekuwa na maoni mbalimbali ya wananchi na vyombo vya habari, lakini Mheshimiwa Rais tunatambua kwamba sisi viongozi wa dini zote tuliomba kuja kukuona pale mwanzoni na ulitupokea na tulikuletea maoni yetu kama viongozi wakuu wa dini, ukaahidi kuwa maoni yatafanyiwa kazi, tuna imani na wewe"  alisema Askofu Dkt. Fredrick Shoo

Askofu Dkt. Shoo pia amesema anatambua kuwa Rais Dkt. Samia alipokea kijiti cha uongozi katika mazingira magumu sana, lakini pamoja na mazingira yale alianza historia mpya ya nchi kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Urais jambo ambalo wengi hawakuamini na mpaka leo wamebaki na jinamizi la namna hiyo, na kwamba huo ulikuwa mpango wa Mungu.

"Najua katika jambo hilo linaelekea mahali tunataka kugawanyika kabisa, wengine wanatumia sababu za kidini, wengine wana maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi, nashukuru Mungu amekujalia hekima kama mama na kiongozi, umekaa kimya" -  Askofu Dk Fredrick Shoo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT). 

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mgeni rasmi katika madhimisho ahayo, amesema Serikali itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zote zinazojitokeza katika ushirikiano uliopo chini ya sera ya PPP, ili kuendelea kumuhudumia mwananchi  na kwamba hakuna jambo lisilokuwa na changamoto lakini zinapojitokeza zinapaswa kufanyiwa kazi kwa pamoja ili ziondoke.

"Nimeyasikia yote uliyoyasema kuhusu usalama, amani, umoja na muendelezo wa taifa letu, niliamua kunyamaza kimya, na naendelea kunyamaza kimya, nachotaka kuwahakikishia hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa taifa hili, na hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuuza taifa hili, na hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuharibu amani na usalama kwenye taifa letu" - Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika maadhimisho hayo ya miaka 60 ya KKKT, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa hakuna mtu mwenye ubavu wa kuligawa, kuuza wala kuharibu amani ya taifa la Tanzania