
Dola ya Marekani
Akizungumza leo Agosti 21, 2023, katika kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma, Gavana wa Benki Kuu Emmanuel Tutuba, amesema Tanzania inatekeleza mikakati ya kuimarisha upatikanaji wa dola hivyo kuendelea kushikilia pesa hizo kuna athari ya kupata hasara badala ya faida.
"Niwaombe wanaoshikilia dola mziweke sokoni katika mfumo ulio rasmi, tutawachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kujihusisha na biashara haramu ya soko la fedha (black market)," amesema Tutuba
Kwa sasa, Tutuba amesema Serikali inapata dola za Marekani kupitia utaratibu wa kawaida ukihusisha mikopo, misaada, mauzo ya nje na kwamba kuna ongezeko la watalii ambao pia wamekuwa wakichangia katika upatikanaji wa dola.
Kwa mujibu wa Gavana, upungufu wa dola ni tatizo la kiduni lililochangiwa na wachapishaji wa fedha hiyo, Marekani, ambayo imeamua kudhibiti mfumuko wa bei kwa kupunguza usambazaji wa dola sokoni.