Sunday , 20th Aug , 2023

Kiongozi wa utawala wa kijeshi nchini Niger Abdourahamane Tchiani ameonya mataifa ya nje kuingilia masuala ya ndani ya taifa hilo.

Tangazo lake hili alilolitoa kupitia televisheni ya taifa Tchiani linajiri baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kusema kuwa viongozi wake wa ulinzi wanapanga kuuingilia mzozo huo iwapo uongozi unaozingatia katiba hautarejeshwa nchini humo. 

ECOWAS ilikubali kutumia “kikosi cha kuingilia kati muda wowote” kama hatua ya mwisho kurejesha demokrasia nchini Niger baada ya majenerali kumuondoa na kumuweka kizuizini rais Mohammed Bazoum hapo tarehe 26 Julai na kuchukua madaraka lakini ilisema inaunga mkono mazungumzo ili kumaliza mzozo huo

Kwa upande mwingine, Tchiani amesema pia ataunda serikali ya mpito itakayokuwa madarakani kwa miaka mitatu.  Hatua hii itatanguliwa na mazungumzo ya kitaifa ndani ya siku 30 kulijadili hilo na Wa-Niger wote. Mazungumzo hayo yatatoa muelekeo wa kuundwa kwa katiba mpya.