Friday , 18th Aug , 2023

Serikali ya Kenya kupitia ofisi ya Msajili wa vyama imefuta usajili wa kanisa la Newlife Prayer la mchungaji Ezekiel Odero.

Taarifa ya msajili wa vyama Maria Nyariki imesema imechukua uamuzi huo kwa kutumia nguvu iliyopewa kisheria katika kifungu cha 12 (1) cha Sheria ya vyama.

Kupitia taarifa ya gazeti la serikali usajili wa makanisa mengine manne pia umefutwa

Makanisa mengine ni Goodnews International Ministries ambalo usajili wake ulifutwa Mei 19, Helicopter of Christ Church ambalo lilifutiwa usajili Mei 19, 2023.

Kanisa la Theophilus lilifutwa Mei 19, pamoja na Kanisa la Kings Outreach

Kanisa la Chama cha Wamiliki wa nyumba za Royal Park Langata ambalo lilisajiliwa kama Jumuiya nalo lilifutwa Juni 19, 2023

Wito wa kudhibiti makanisa umekuwa ukiongezeka huku Naibu Rais Rigathi Gachagua akiwataka viongozi wa kidini kuunga mkono mpango wa serikali wa kukagua kanuni zinazosimamia mashirika ya kidini.

Hatua hizi za kudhibiti na kutathmini upya makanisa zinajiri kufuatia matukio ya watu kulaghaiwa na baadhi ya wahubiri, na kupokonywa mali, wengine kuendesha ibada ya kufunga hadi kufa, ambayo imepelekea vifo vya zaidi ya watu 400 kufikia sasa kule shakahola kaunti ya kilifi.