
Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba
Makubaliano hayo yamefikiwa Mjini Beijing-China, wakati wa ziara ya ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambapo ujumbe huo, pamoja na mambo mengine, una lengo la kuimarisha uhusiano na taasisi za fedha za China ili kupata fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa nchini.
Dkt. Nchemba amesema kuwa ushirikiano huo utaimarishwa kupitia nyanja za uwekezaji, biashara pamoja na mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Amesema kuwa hatua hiyo ni matokeo ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini China aliyoifanya Mwezi Novemba mwaka jana ambapo katika mazungumzo yake na Rais wa China-Mhe. Xi Jimping walikubaliana kukuza mahusiano ya kiuchumi katika nyanja mbalimbali.
Dkt. Nchemba alibainisha kuwa mazungumzo na taasisi hiyo yataiwezesha Serikali na kampuni za Sekta Binafsi kupata dhamana kutoka kwa taasisi ya SINOSURE ili kupata mikopo kutoka kwa taasisi za fedha za China.
Ameeleza kwamba hatua hiyo itasaidia wawekezaji wa China kwenda kuwekeza Tanzania mitaji na teknolojia ambazo zinatasaidia kuharakisha maendeleo ya wananchi na kukuza uchumi kwa ujumla. Vilevile hatua hiyo itawezesha kampuni za China kuuza kwa kampuni za Tanzania bidhaa mbalimbali kwa mkopo kupitia dhamana ya taasisi ya SINOSURE.
“Mazungumzo yetu yamekwenda vizuri na sasa wataalam wa pande zote mbili wameanza majadiliano namna Tanzania inavyoweza kupata fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa njia ya treni ya kisasa-SGR, vipande namba tano hadi saba vinavyoanzia Isaka-Mwanza-Tabora–Kigoma-Uvinza hadi Malagarasi, kwenda hadi nchi Jirani za Burundi na Congo DRC," amesema Waziri Nchemba