Thursday , 3rd Aug , 2023

Dereva aliyegonga na kusababisha vifo vya wakimbia jogging sita na majeruhi tisa mkoani Mwanza Osward Kaijage, amefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza na kusomewa shtaka moja lenye makosa 15 huku mahakama hiyo ikimuachia kwa dhamana.

Gari lililosababisha ajali

Mwendesha Mashtaka wa serikali Anitha Mweri, na Mwanahawa Changale wameiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka moja la kuendesha gari kwa spidi kubwa na kupelekea vifo vya watu sita na kujeruhi.

Baada ya kusomewa shtaka na makosa yanayomkabili mshtakiwa huyo alikana makosa hayo na upande wa serikali ukaomba ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kusoma hoja za awali kufuatia upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Amri Linus na Steven Kitale ukaiomba mahakama kumpa dhamana mshtakiwa huyo wakitoa sababu tano ikiwemo mshtakiwa huyo kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi tangu ajali ilipotokea, pia mshtakiwa huyo kuugua na kuendelea na matibabu hospitalini yaliyotokana na ajali hiyo, aidha yupo tayari kufuata masharti ya dhamana yatakayotolewa katika mahakama hiyo.

Hakimu mkazi wa mahakama hiyo ya wilaya ya Ilemela Amani Sumari baada ya kupitia hoja za pande zote mbili ikiwemo hoja ya upande wa mashtaka iliyotaka vigezo vya dhamana vizingatie ukubwa wa makosa akasema dhamana ya mshtakiwa huyo ipo wazi na kutakiwa kuwa na wadhamini wawili mmoja akiwa mfanyakazi wa serikali na kusaini bondi ya shilingi milioni kumi kila mdhamini.

Mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana na kesi yake itatajwa tena Agosti 10 2023 kwa ajili ya hoja za awali.