Msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka kundi la Chamber Squad, Moses Frank Mshangama maarufu kwa jina la 'Mez B' amefariki dunia asubuhi ya leo huko mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mama yake mzazi mchungaji Marry Mkandawile inasema kuwa Mez B alikuwa akisumbuliwa na maambukizi katika mapafu na uti wa mgongo kwa muda mrefu, maradhi ambayo huenda ndiyo yaliyosababisha kifo chake.
Mchungaji Marry Mkandawile amesema kuwa Mezi B alianza kusumbuliwa na maradhi hayo mwishoni mwa mwaka jana akiwa Dar es salaam, ambapo baada ya hali kujirudiarudia, familia yake iliamua kumhamishia nyumbani kwao mjini Dodoma mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana kwa matibabu zaidi.
Mez B anakuwa ni msanii wa Pili kufariki dunia kutoka katika kundi hilo katika kipindi cha miaka miwili baada ya Albert Mangwea aliyefariki mwezi Mei mwaka 2013.
Maziko yatafanyika siku ya Jumatatu (Februari 23) nyumbani kwao maeneo ya Kisasa mjini Dodoma.
EATV inatoa pole kwa familia ya marehemu na wote wale wanaoguswa na msiba huo kwa namna moja ama nyinine.