Friday , 9th Jun , 2023

Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka sekta binafsi nchini kukaa kwa pamoja ili vitengo vyao visomane huku akisema kuwa ana wasiwasi kuwa kuna tatizo

Rais Samia amesema hayo wakati akifungua na kushiriki Mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) katika Ukumbi wa Kikwete - Ikulu Dar es Salaam leo tarehe 09 Juni, 2023

Ameeleza kuwa ni kweli serikali na sekta za umma wamekubali kuwa kuna tatizo la mifumo kusomana na lifanyiwa kazi kwa haraka sana lakini ni wazi kuwa hata sekta binafsi kuna tatizo na sekta zao kutosomana

"Kazi kubwa inaendelea kufanyika ya kuboresha mifumo ya TEHAMA, mifumo yetu haisomani, taarifa hazioani, kazzi tunayokwenda kuifanya kwa nguvu kubwa sasa ni kufanya mifumo ndani ya sekta ya umma isomane, lakini pia iwe na vigezo vya kimataifa"

"La mwisho nalotaka kuzungumza na sekta binafsi ni uhusiano kati yenu, sisi tumekubali sekta zetu tuna udhaifu hazisomani, lakini nina wasiwasi na ndani ya sekta binafsi vitengo vyenu havisomani, wale wanasema lile hawa wanasema lile, tunaomba nanyi mkanyooshane"

Aidha Rais Samia katika Mkutano huo amewaagiza viongozi wote wa ngazi za mikoa na wilaya kuendeleza majadiliano kupitia nabaraza ya biashara na kuwasilisha ripoti kila baada ya robo ya mwaka

"Nichukue nafasi hii kuwaagiza viongozi wote ngazi zote, kuendeleza majadiliano kupitia mabaraza ya biashara ya mikoa na wilaya na kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji katika maeneo yenu, na kuwasilisha taarifa za utendaji wa mabaraza hayo kila robo mwaka na wanaofanya vizuri tutawazawadia" 

Katika hatua nyingine Rais Samia amesema kuwa kukua kwa pato la taifa nchini ni kutokana na mazingira mazuri yaliyopo ya biashara na uwekezaji 

"Kama mnavyofahamu kwamba pato la taifa katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka jana tu liliongezeka kufikia trilioni 45.2 kutoka shilingi trilioni 39.9 mwaka 2021, mafanikio haya ni matokeo ya maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia sera, sheria, kanuni na taratibu zetu hapa nchini"