Wednesday , 17th May , 2023

Timu ya Yanga nchini, imepongezwa kwa kazi kubwa ya kujituma na kuiletea heshima Tanzania kimataifa kwa kuifunga timu ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa goli 2-1 kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kutinga fainali, jitihada hizo zinatambulika kuwa ni Uzalendo wa hali ya juu. 

Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Lwoga na kulia ni wachezaji wa Yanga

Akiungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipongeza timu ya Yanga, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Lwoga amesema kuwa, ushindi huo wa timu ya Yanga umepatikana wakati dunia inasherehekea Siku ya Makumbusho Duniani ifikapo Mei 18 kila mwaka.

Timu hiyo imekuwa mdau mkubwa wa Makumbusho ya Taifa kwa kutembelea na kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo uzalendo lakini pia kuhifadhi vitu muhimu ambavyo ni urithi wa kihistoria wa Timu hiyo kubwa nchini.

Dkt. Lwoga ametoa wito kwa timu zingine kushirikiana na Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika kuwapatia elimu ya uzalendo, histori ya Tanzania na uhifadhi wa urithi wa historia ya timu hizo kama zinavyo fanya timu ya Simba na Yanga.

Siku ya Makumbusho Duniani ilianzishwa na Baraza la Makumbusho Duniani (ICOM) mwaka 1977.