
Usiku wa kuamkia leo Ijumaa kumetolewa taarifa za kutia moyo kuhusu mzozo wa Sudan. Taarifa zimearifu kuwa pande hasimu kwenye mzozo huo zimekubaliana kuwalinda raia na kuhakikisha huduma za msaada wa kiutu zinafika kwenye maeneo yenye uhitaji bila vizingiti.
Licha ya hatua hiyo, pande hizo mbili hazijakubaliana bado kusitisha mapigano wala kutafuta mkataba mpana wa kumaliza vita.
Maafisa wa Marekani waliokaririwa na Shirika la Habari la Associated Press wamesema maafikiano ya kumaliza vita ni jambo ambalo bado haliko karibu.
Baada ya wiki nzima ya majadiliano katika mji wa mwambao wa Jeddah nchini Saudi Arabia, kile kilichopatikana ni pande hizo mbili hasimu kutia saini azimio la kuonesha dhamira ya kufanya kazi pamoja ili kupata makubaliano mapya ya kusitisha vita kwa muda mfupi.
Azimio hilo linatilia mkazi umuhimu wa kila upande kusaidia upatikanaji huduma muhimu za kiutu na kuwalinda raia. Pia linatoa mwito wa kurejeshwa huduma ya nishati ya umeme, maji na nyingine muhimu.
Vikosi vya pande hasimu pia vinatakiwa kuondoka kutoka kwenye majengo ya hospitali na kila upande uruhusu kufanyika mazishi ya heshima kwa wale waliopoteza maisha.