Mkuu wa wilaya ya Bahi Betty Mkwasa
Mkuu wa wilaya ya Bahi Betty Mkwasa ametoa siku Tano kwa watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu kwenda kidato cha Kwanza wilayani humo wanaripoti shuleni mara moja huku akiagiza kamati ya huduma za jamii kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wazazi au walezi watakao bainika kuhusika na utoro wanafunzi.
Ametoa tamko hilo wakati akizindua mfuko wa elimu wa wilaya hiyo wenye lengo la kusaidia kuwasomesha wanafunzi ambao hawana uwezo unaoendeshwa na kamati ya madiwani ya huduma za jamii kwa kukusanya fedha kutoka kwa wananchi wilayani humo kupitia njia mbalimbali ikiwemo vibali vya kupeleka ng’ombe mnadani.
Amesema hadi hivi sasa asilimia 39 ya wanafunzi waliofaulu hawajafika shuleni huku wengine wakiwa wameshaingizwa katika mpango huo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mfuko huo wa elimu ambaye pia ni diwani wa kata ya lamaiti, Dornald Mejiti amesema mfuko huo kwa sasa una shilingi million 30 ambazo wameanza nazo kwa kusomesha watoto 426 kwa wilaya nzima ambapo wanawalipia ada, kuwanunulia sare za shule, viatu na madaftari.
Katika shule ya sekondari Bahi ambapo ndipo uzinduzi umefanyika mfuko huo unasomesha wanafuzi 40 ambapo mpaka sasa waliofika shuleni ni 24 tu huku wanafunzi 16 wakiwa hawajaripoti.
Naye mwanafunzi Anna Chipengwa mmoja kati ya wanufaika wa mfuko huo ametoa rai kwa wazazi ambao watoto wao wanasomeshwa kuwahimiza kusoma kwa bidii ili waweze kuwakwamua katika umasikini.