Inaelezwa kuwa wawili hao walikuwa marafiki na siku ya tukio hilo Oktoba 24/2022 walienda pamoja kunywa pombe na waliacha supu nyumbani ambapo Mtepa aliwahi kurudi nyumbani na kuamua kuinywa supu hiyo
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mchakama, Mohamedi Waziri Mpinga amesema marehemu Mtepa na Akadwii ni marafiki na walikuwa na tabia ya kutembeleana na muda mwingine kila mmoja alikuwa analala kwa mwenzake
“Huyu jamaa amemkata kichwa chote na kuacha sehemu kidogo ya ngozi kutenganisha kati ya kichwa na kiwiliwili”Alisema Mpinga.
Mpinga alisema siku hiyo ya Oktoba 24/2022,marafiki hao walikwenda kunywa Pombe, huku nyumbani kwao waliacha supu,hivyo Mtepa aliamua kurudi nyumbani kulala, huku akimuacha mwenzake akiendelea kunywa Pombe.
Alisema baada ya kufika Nyumbani Mtepa alichukuwa supu ya Ng’ombe na kuinywa kisha kulala usingizi, ambapo Akadwii aliporejea na kuangalia supu bila ya kuikuta, inaelezwa alichukuwa gongo na kumpiga Mtepa kichwani, hali iliyomstua usingizini na kuanza kugalala.
Mwenyekiti huyo wa Kijiji cha Mchakama akasema baada ya kuona hivyo, Akadwii alichukuwa kisu na kumchinja kwenye shingo misili ya kuku, huku akiwa amebakisha kiasi kidogo cha ngozi kutenganisha kichwa na kiwiliwili.
Alisema mtuhumiwa baada ya kutekeleza unyama huo, alivua nguo za marehemu na kuzivaa yeye kasha kuuchukuwa mwili na kwenda kuutelekeza kwenye mto Mavuji, huku miguu ikiwa ndani ya maji na kichwa nchi kavu.
Mwenyekiti huyo wa alisema wakati Akadwii akirejea nyumbani kwake, njiani alikutana na mtu mmoja bila kumtaja jina na alipomuona nguo alizovaa zimechafuka damu alimuuliza, lakini hakupewa jibu hali iliyomlazimu mwananchi yule kuelekea anakotokea mtuhumiwa na kuukuta mwili huo.
“Huyu ndugu baada ya kuukuta mwili wa Mtepa upo kwenye mto Mavuji alitoa taarifa kwa uongozi wa Kijiji cha Mavuji”Alisema Mpinga.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mavuji,Shaibu Mnula na mwenyekiti Issa maji,wamekiri kupata taarifa hiyo na walipofuatilia waliukuta mwili huo ukiwa umetelekezwa Mtoni,huku miguu ikiwa ndani ya maji eneo kavu.
Walisema kufuatia tukio hilo,walipiga simu kituo cha Polisi Wilaya,ambapo askari wakiongozana na mtaalamu wa Afya walifika kuona hali hiyo na kutoa ruhusa kwa ndugu na jamaa kuuzika mwili huo.
Hata hivyo taarifa kutoka kwa viongozi wa kijiji cha Mavuji inaeleza tayari Akadwii amekamatwa na anashikiliwa na Serikali ya Kijiji hicho, tayari kumkabidhi kwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria.
Kamanda wa Polisi Mkoani Lindi, Pili Mande alipoulizwa juu ya tukio hilo, amekiri kulipata na amesema tayari amewatuma vijana wake kwenda kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo na kumchukuwa mtuhumiwa kwa ajili ya taratibu zingine za kisheria.