Thursday , 20th Oct , 2022

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja amewataka watanzania kuacha kuamini kuwa utalii ni kwa ajili ya wageni pekee, na kuwahimiza kushiriki katika shughuli za utalii ili kuongeza pato la taifa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja

Naibu Waziri Masanja ameyasema hayo leo, alipotembelea mabanda mbalimbali kuelekea maonesho ya 6 ya kimataifa ya Kiswahili yanayotarajiwa kuanza Oktoba 21 hadi 23 mwaka huu, Mlimani City jijini Dar, huku akisisitiza kuwa Utalii umekuwa chanzo cha ajira kwa watanzania wengi.

Aidha Naibu Waziri Masanja amesema maonesho hayo ni muendelezo wa hamasa inayotokana na Filamu ya Royal Tour, ambayo imechochea kukua kwa kasi kwa sekta ya utalii. 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Felix John ameeleza kuwa maonesho haya yalitakiwa kufanyika mwaka 2019 lakini yalikwamishwa na janga la UVIKO- 19 lakini kwa sasa maonesho haya yatakuwa nyenzo katika kuendelea kuitangaza Tanzania Kimataifa.

Kwa upande wao vijana wanaojishughulisha na utalii, wamewataka vijana wenzao kuacha kulalamika kwa kukosa ajira na badala yake watumie fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya utalii.