Thursday , 14th Jul , 2022

Shirikisho la mpira wa miguu duniani (FIFA) limetoa siku 45 kwa klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco kumlipa fidia ya fedha mchezaji wao wa zamani Simon Msuva kiasi cha shillingi bilioni 1.6 kutokana na kushindwa kumtimizia matakwa ya kimkataba.

Simon Msuva

Akizuñgumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,mshauri wa Saimon Msuva, Bi Yasmin Razak amesema mbali na FIFA kutoka siku 45 kulipwa madai ya fedha zake lakini pia wametoa siku 10 kwa Wydad kukata rufaa juu ya maamuzi ya kesi hiyo

"Wachezaji wanapaswa wasiwahofie mawakala watambue wanaishi kupitia migongo yao vile vile ninaomba TFF waratibu mawakala ambao wamesajiliwa ili wachezaji wetu wasipate shida kama alizozipata Msuva iwajengee wachezaji mazingira ambayo hata wakiachana na mpira wanakuwa wamefaidika kupitia mpira''amesema Yassin Razak.

Kwa upande wa mchezaji Saimon Msuva amewataka wachezaji wenye ndoto za kucheza soka la kulipwa kutafuta mawakala wazuri wa kuwasimamia pamoja na kupambania haki zao za kimkataba na vilabu wanavyosajiliwa navyo.

" Kilichonikuta walinipa makaratasi mengi ya kusaini ambayo yalikuwa yameandikwa kwa lugha ya kifaransa nilisaini sikujua kile ambacho kitanikuta sitaki kuwasikia waarabu nimeteseka mno''amesema mchezaji huyo.

Saimon Msuva alisajiliwa na Wydad Casablanca akitokea klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco msimu wa 2020/21 huku kesi yake ikichukua miezi saba kutokana na kutolipwa fedha zake za usajili ndani ya klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco.