Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. Christopher Kangoye, akizungumza na wadau mbalimbali.
Akithibitisha kutokea kwa moto huo mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye alisema kuwa wamelazimika kuwahamishia wasichana hao katika mabweni ya chuo cha ualimu Mpwapwa kutokana na moto huo kuteketeza kila kitu kilichokuwemo ndani ya bweni lao.
Mkuu wa shule hiyo Nelson Milanzi amesema kuwa moto huo ulianza majira ya saa 3:20 jana asubuhi wakati wanafunzi hao wakiwa madarasani ambapo moto huo uliteketeza kila kitu kilichokuwemo bwenini na kuwaacha wanafunzi hao wakiwa hawana mahali pa kulala wala nguo za kubadilisha.
Hata hivyo chanzo cha moto huo bado hakijajulikana ambapo kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma amesema kuwa jeshi hilo inashirikiana na shirika la umeme wilayani humo ili kujua chanzo cha moto huo, na hakuna taarifa za kifo zilizoripotiwa katika tukio hilo.