Kocha Jose Mourinho
PSG ina mpango wa kumfuta kazi kocha wake Mauricio Pochettino siku chache zijazo, baada ya kocha huyo raia wa Argentina kushindwa kukiongoza kikosi hicho kutwaa ubingwa wa klabu bingwa barani Ulaya (UEFA Champions League).
Kutoka Italia hii leo zimeripotiwa kuwa Jose Mourinho hana mpango wa kuondoka AS Roma anataka kumalizia kazi aliyoanza kuifanya msimu uliopita. Mourinho amebakiza miaka 2 kwenye mkataba wake na Roma na msimu uliopita 2021-22 amekiongoza kikosi hicho kuchukua ubingwa wa michuano ya Europa Conference League ambalo ni taji la kwanza kwa klabu hiyo kushinda baada ya miaka 14.
Makocha Jose Mourinho na Zinedine Zidane ndio wanaopigiwa upatu kuwa mmoja wao anaweza kupewa kibarua cha kukinoa kikosi hicho cha matajiri wa jiji la Paris. Makocha hawa wanapewa kipaumbele kutokana na mafanikio waliyoyapa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya.
Zidane ambaye ameshinda ubingwa wa klabu bingwa ulaya mara 3 akiwa na Real Madria anatajwa kuwa hana nia kukubali kibarua hicho kwani kwa sasa nia yake ni kutaka kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ufaransa. Hivyo kocha pekee ambaye PSG wanaamini anaweza akawapa ubingwa wa Ulaya ni Jose Mourinho ambaye ameshinda ubingwa wa michuano hiyo mara 2 akiwa na vilabu viwili tofauti ambavyo ni FC Porto na Inter Milan.


