Monday , 6th Jun , 2022

Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani Bernard Membe, ameitolea ufafanuzi kauli iliyotolewa na Waziri wa Habari Nape Nnauye, siku aliyokuwa anakabidhiwa kadi yake ya CCM na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hichio Shaka Hamdu Shaka iliyosema "Bahari imetulia, Mwenyezi Mungu ameamua ugomvi".

Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani Bernard Membe,

Akitolea ufafanuzi wa kauli ya Waziri Nape, Mhe. Membe amesema kuwa kauli hiyo ililenga kuwaeleza wananchi wa Tarafa ya Rondo aliokuwa na ugomvi nao kwamba sasa umemalizika, kwani kufukuzwa kwake ndani ya CCM kuliibua hasira miongoni mwa wananchi, hatua ambayo ilisababisha katika moja ya mkutano wa Nape kuhudhuriwa na watu 12 pekee.

"Kwa sababu watu walikuwa na hasira na wakabishana pale, mimi mwenyewe sikuwepo, nilipata tabu sana kama mbobevu, kama mstaafu, kama mtu ambaye anamshabikia Nape Nnauye, sasa tumekwenda na hiyo misuguano hadi niliporejea CCM," amesema Membe.

Mei 29 mwaka huu, Membe alikabidhiwa kadi yake ya CCM baada ya hapo awali kufukuzwa uanachama na kisha baadaye kusamehewa na Rais Samia, na baada ya kurejea ndani ya chama chake cha zamani, Membe alizungumza na wananchi huku akiwasihi yaliyopita wayaache na wagange yajayo.

"Nilimtaka Nape alieleze hilo, sasa Nape ni msomi na mwanasiasa, akaliweka kwa lugha aliyoliweka, kwahiyo wananchi wa Rondo kauli ya Nape ni ya kueleza kwamba mgogoro wa wananchi wa Rondo na mbunge ambao walikuwa nao sasa umekwisha hiyo ndiyo tafsiri tuliyoipata," amesema

Miaka miwili akiwa nje ya CCM, Membe aligombea Urais wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo alichojiunga nacho Julai 15, 2020 miezi kadhaa baada ya kufukuzwa CCM.