
Azam FC itakua nyumbani Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam, kuikaribisha Young Africans ambayo mpaka sasa haijapoteza mchezo tangu ilipoanza msimu huu 2021/22.
Ajibu amesema Azam FC imejiandaa kikamilifu kuelekea mchezo huo, huku wakitarajia kupambana na kupata ushindi katika Uwanja wao wa nyumbani, ili kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 walipokutana na Yanga, Uwanja wa Benjamin Mkapa katika Duru la Kwanza la Ligi Kuu msimu huu.
Hata Hivyo Kiungo huyo wa zamani wa Simba SC, amekiri wazi kuwa Yanga ina kikosi kizuri na imara, lakini bado anaamini Azam FC ina kikosi imara zaidi na ndio maana hana shaka na alama tatu za kesho Jumatano (April 06).
“Tunajua kama Young Africans ni timu nzuri na inaongoza msimamo wa ligi, lakini tumejipanga kukabiliana nayo na kuchukua alama zote tatu,” amesema Ajibu ambaye pia amewahi kuichezea Yanga.
Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 48 baada ya michezo 18 huku Azam FC ikishika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama zake 28, saba nyuma ya Simba SC iliyopo nafasi ya pili.